Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiongozi wa zamani wa Ivory Coast apanda kizimbani kwa mara ya kwanza

Kiongozi wa zamani wa Ivory Coast apanda kizimbani kwa mara ya kwanza

Kiongozi wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo amepanda kizimbani kwa mara ya kwanza Jumatatu Desemba 5 kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC. Gbagbo ambaye pia ni Rais wa kwanza kufikishwa mahakani hapo alionekana mtulivu na kutabasamu kwa wafuasi wake wakati wa dakika 25ambazo majaji walikuwa wakimsomea mashitaka yake. Gbagbo mwenye umri wa miaka 66 amewaambia majaji hawana haja ya kusoma mashitaka dhidi yake.

Anashitakiwa kwa kubeba jukumu binafsi la uhalifu dhidi ya ubinadamu uliotekelezwa baada ya uchaguzi mkuu nchini Ivory Coast mwaka 2010. Uhalifu huo unajumuisha mauaji, ubakaji na mifumo mingine ya ukatili na vitendo visivyo vya kibinadamu.

Waendesha mashitaka wanasema watu 3000 wameuawa baada ya ghasia zilizozuka kutokana na Gbagbo kutokubali kushindwa katika uchaguzi. Mahakama ya ICC baada ya kumsomea mashitaka yake imesema kesi kamili ya mashitaka dhidi ya Gbagbo itaanza kusikilizwa Juni 18 mwaka 2012.