Kenya imelitaka Baraza la Usalama kutafuta njia ya kurejesha utulivu Somalia

1 Disemba 2011

Rais Mwai Kibaki wa Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta haraka njia za kurejesha utulivu Somalia.

Akizungumza kwenye mkutano wa 13 wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mjini Bujumbura Burundi Rais Kibaki amesema azimio la kurejesha utulivu Somalia linahitajika haraka. Amesema machafuko ya Somalia yanaendelea kusambaa na kusababisha usalama mdogo ndani ya taifa hilo na nchi jirani na tatizo la usalama Somalia ni suala la kimataifa na hivyo Baraza la Usalama linatakiwa kufanya kila liwezekanalo kurejesha utulivu Somalia taifa lililokuwa vitani kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Jean Ping, wanadiplomasia, wadau wa maendeleo, maafisa wa ushirikiano wa nchi za Afrika ya Mashariki, maafisa wa soko la pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika COMESA na maafisa wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter