UM wataka kutekelezwa kwa uzazi wa mpango wa hiari

30 Novemba 2011

Viongozi wa dunia wametolewa mwito kuupa msukumo mpango wa utelezaji uzazi wa mpango wa hiari, kwa madai kwamba kuwekeza kwenze uzazi wa mpango siyo tu kunaimarisha hali ya maisha wanawake na watoto lakini pia ni njia tosha ya kukabiliana na tatizo la umaskini.

Akizungumza kwenye kongamano la kimataifa la uzazi wa mpango huko Dakar, Senegal, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu UNFPA,  Babatunde Osotimehin, amesema kuwa bado kuna hali ya kusua sua juu ya utekelezaji mipango inayoangazia uzazi wa mpango kwa hiari.

Amewataka viongozi wa dunia kugeukia miradi inayoangazia uzazi wa mpango na kuongeza kuwa kutimizwa kwa miradi hiyo kutatoa fursa nzuri kwa historia ya dunia ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto la ongezeko la watu.

Pia ameweka zingatio juu ya kunusuru maisha ya kina mama na watoto akisema kwamba uzazi wa mpango ni habari njema kwa kina mama ambao wakati mwingine wanakumbana na matukio ikiwemo vifo kutokana na uzazi wa mfululizo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud