Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya za kiraia zaunga mkono mpango wa amani Somalia:Mahiga

Jumuiya za kiraia zaunga mkono mpango wa amani Somalia:Mahiga

Mkutano wa siku tatu wa wawakilishi wa jumuiya za kijamii umemalizika mjini Moghadishu kwa washiriki kuelezea uungaji mkono wake mpango wa amani wenye lengo la kumaliza kipindi cha mpito ambapo serikali ina jukumu kubwa katika miezi tisa nchini Somalia.

Mkutano huo wa Jumiya za kiraia ulioanza Novemba 26 hadi 28 umewahusisha wawakilishi 60 ambao ni viongozi wa dini, viongozi wa koo, jumuiya ya wafanya biashara, watu waishio nje ya nchi, vijana na makundi ya wanawake.

Mkutano huo umewezeshwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya siasa kwa ajili ya Somalia UNPOS na umewajumuisha pia wawakilishi wa taasisi za serikali ya mpito, uongozi wa Puntland na Galmudg na Ahlu Sunnah Wal Jamaa.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Somalia balozi Augustine Mahiga akizungumza wakati wa mkutano huo amewaambia washiriki kwamba ana matumaini makubwa kutoka kwao kwani uwepo wao kwenye mkutano ni hatua muhimu, kwani jumuiya za kijamii ni daraja kati ya tofauti za kisiasa na kwamba uwezo wa kufanikisha hali hiyo upo mikononi mwa jumuiya hizo.

Makundi hayo yametoa mapendekezo mwishoni mwa mkutano na yanajumuisha kuongeza msaada wa fedha ili kutekeleza mipango ya usalama, kuheshimu muda uliowekwa wa kukamilisha mpango wa mpito, kuidhinisha katiba, kusaidia mabadiliko ya bunge, kuunda tume ya kweli na maridhiano, kufanya mikutano ya upatanisho na kuanzisha sheria ya kupambana na ufisadi.