Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria inatekeleza uhalifu dhidi ya binadamu:UM

Syria inatekeleza uhalifu dhidi ya binadamu:UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea hofu yake kutokana na kuendelea kwa machafuko na ongezeko la vifo nchini Syria.

Hofu hiyo imekuja wakati leo Jumatatu ripoti ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa imetoka ikishutumu majeshi ya usalama ya Syria kutekeleza uhalifu wa binadamu dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Tume huru ya uchunguzi imewasilisha ripoti hiyo kwa baraza la haki za binadamu ambayo ina madai ya mauaji, ukiukaji wa haki za watoto na vitendo vya ubakaji.

Tume hiyo imesema imewahoji waathirika 223, mashahidi na walioasi jeshi wakati ikichunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu kuanzia mwishoni mwa septemba hadi katikati ya Novemba 2011.

Zaidi ya watu 3500 wameripotiwa kuuawa katika machafuko hayo yaliyoanza mwezi Machi.