Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR aonya juu ya watu kutawanya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa

Mkuu wa UNHCR aonya juu ya watu kutawanya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Antonio Guterres leo amelitahadharisha baraza la usalama kuhusu kuongezeka kwa tishio la amani na usalama wa kimataifa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na muingiliano wa sababu zingine zinazowatawanya watu.

Akizungumza kwenye Baraza la Usalama Guterres amesema mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa yakichochea kiwango na ukubwa wa mtawanyiko wa watu duniani. Pia ametoa tahadhari ya kuliangalia suala la mabadiliko ya hali ya hewa kipekee kando na masuala mengine ya kimataifa kama ongezeko la watu, kukua kwa miji na ongezeko la upungufu wa chakula, maji na nishati.

Gutteres ameelezea uwezekano wa kushuka kwa kilimo katika nchi zinazoendelea na kugombea rasilimali chache zitakazokuwepo ikiwemo maji, na ardhi ya kilimo. Amesema kuna ongezeko la ushahidi wa uhusiano baina ya mabadiliko ya hali ya hewa na mafuriko na pia majanga mengine ya asili ambayo yanakadiriwa kuwatawanya watu zaidi ya milioni 40 mwaka 2010 pekee.