Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

November 20 ni siku ya kimataifa ya haki za mtoto:UNICEF

November 20 ni siku ya kimataifa ya haki za mtoto:UNICEF

Katika maadhimisho ya 22 ya mkataba wa kulinda haki za watoto, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limeungana na siku ya salama na kuchukua hatua za kuwalinda watoto duniani kuzindua mpango mpya wa miaka mitatu kwa zaidi ya mataifa 30 wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na ghasia.

Siku ya salama na kuchukua hatua kwa ajili ya watoto ni vuguvugu linaloshajihisha jukumu linaloweza kuchukuliwa na jumuiya za kidini katika kuwalinda watoto kwa kuchagiza hatua kama za kuorodheshwa wakati wa kuzaliwa, malezi bora na kupinga hatua ambazo zinakiuka haki zao au kuwaumiza watoto mfano ndoa za utotoni.

UNICEF inasema wakati hatua zimepigwa katika kupunguza vifo vya watoto na kuboresha afya duniani kote, mamilioni ya watoto wako katika hatari ya kukabiliwa na ghasia na ukatili.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa UNICEF Athony Lake amesema msukumo wa siku ya kimataifa ya haki za watoto mwaka huu ni ndoa za utotoni ambazo zinaathiri wasichana wengi.

Amesema wasichana hao wanaoolewa wakiwa wadogo sana wanakuwa katika hatari ya kunyanyaswa, kutendewa ukatili na kunyonywa pia wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa kuliko wanawake waliopevuka.