Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kuvumiliana iwe zaidi ya kuishi pamoja kwa amani:Ban

Hali ya kuvumiliana iwe zaidi ya kuishi pamoja kwa amani:Ban

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuvumiliana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hali ya kuvumiliana ni muhimu sana na ni lazima iwe zaidi ya kuishi kwa pamoja kwa amani. Amesema ni lazima iwe ni maelewano yanayopatikana kwa njia ya mazungumzo na ushirikiano na wengine.

Akisisitiza umuhimu wa kufanya hivyo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Nassir Abdulaziz Al-Nasser amesema ugumu wa changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa unahitaji kuheshimiana, kuelewana na kuthaminiana baina ya watu, familia na jamii.

Na ili kufanikisha azima hiyo uwazi, kusikizana na mshikamano vinahitajika, na juhudi kubwa zinapaswa kufanywa hasa katika kuelimisha watoto kuhusu kuvumiliana, haki za binadamu, mahusiano ya matabaka, mila na utamaduni na njia za maisha za watu wengine.

Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO Irina Bokova akitoa ujumbe kuhusu siku hii amesema katika dunia ambayo imeungana kuliko wakati mwingine wowote kutovumiliana hakuna nafasi. Mchanganyiko wa mataifa, utamaduni, jamii unaitaka dunia kuweza kusahau tofauti zao na kuishi pamoja kwa amani na usalama.