Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 440,000 wametawanywa na waasi wa Uganda wa LRA nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Watu 440,000 wametawanywa na waasi wa Uganda wa LRA nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mashambulizi ya waasi wa Uganda wa Lord’s Resistance Army au LRA yamewalazimisha watu takribani 440,000 kuzikimbia nyumba zao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, amesema mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.

Abou Moussa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameyasema hayo akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama kuhusu shughuli za LRA leo Jumatatu. Amesema kundi hilo la waasi linaendelea kuwatia hofu watu katika maeneo ya vijijini ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.

Amesema kwa miaka kadhaa sasa mashambulizi ya LRA dhidi ya raia yamesababisha vifo, utekaji, uporaji, na malaki ya watu kufunga virago au kuwa wakimbizi. Amesema ingawa kundi hilo halina ajenda ya kisiasa, limeendelea kukiuka haki za kimataifa za binadamu na kuogofya watu.

Ameongeza kuwa juhudi za serikali ya Uganda kuafikiana amani na kundi la LRA ambalo pia limekuwa likisumbua Waganda Kaskazini mwa nchi hiyo zimeshindwa kuzaa matunda na kiongozi wa LRA Joseph Kony bado hajakamatwa.