Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanachama wa UM wachagua majaji wa mahakama ya kimataifa ya haki:ICJ

Wanachama wa UM wachagua majaji wa mahakama ya kimataifa ya haki:ICJ

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama leo Alhamisi limewachagua majaji wane watakaofanya kazi kwenye mahakama ya kimataifa ya haki (ICJ) ambayo ni chombo cha kisheria cha Umoja wa Mataifa.

Baada ya duru kadhaa za upigaji kura kwenye Baraza Kuu na Baraza la Usalama Giorgio Gaja kutoka Italia, Hisashi Owanda kutoka Japan, Peter Tomka kutoka Slovakia na Xue Hangin kutoka Uchina wamechaguliwa kushika hatamu kwa muhula wa miaka 9 kwenye mahakama hiyo ya ICJ kuanzia tarehe 5 Februari mwakani.

Kisha kura zikaanza tena kwenye Baraza Kuu na Baraza la Usalama kujaza nafasi ya mwisho ya wajumbe 15 wa ICJ mahakama ambayo pia hujulikana kama mahakama ya dunia yenye makao yake mjini Hague Uholanzi. Wagombea wanapaswa kupata kura za walio wengi kwenye Baraza Kuu na kwenye Baraza la Usalama.

Majaji huchaguliwa kutokana na taaluma na sio utaifa, lakini hairuhusiwi majaji wawili kutoka kwenye taifa moja. Juhudi hivi sasa zinafanyika kuhakikisha mifumo muhimu ya kisheria duniani inawakilishwa katika mahakama hiyo.

ICJ iliyoanzishwa mwaka 1945 ina jukumu la kumaliza mivutano baina ya mataifa na kutoa ushauri katika masuala ya kisheria ambayo yamewasilishwa katika mahakama hiyo na vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa.