Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya upinzani na vifo, AMISOM haitokata tamaa Somalia:Burundi

Licha ya upinzani na vifo, AMISOM haitokata tamaa Somalia:Burundi

Vikosi vya kulinda amani vya muungano wa Afrika ambavyo viko nchini Somalia vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upinzani mkubwa kutoka kwa wanamgambo wa Al-shabaab, vifo wakati mwingine, matatizo ya kiufundi na hata ukosefu wa fedha.

Hata hivyo vikosi hivyo ambavyo kwa sasa vinajumuisha wanajeshi kutoka Uganda na Burundi vikishirikiana na vya serikali ya mpito ya Somalia vimesema havitokata tamaa hadi vitakapokamilisha jukumu lililowapeleka huko. Hivi karibuni wanajeshi kadhaa wa Burundi wameuawa na miili yao kupelekwa nyumbani kwa mazishi.

Taarifa za kutofautia kuhusu idadi ya wanajeshi waliouawa pia zimekuwa zikitanda huku Al-Shabaab wakidai ni 70 na jeshi la serikali likisema sio zaidi ya 10. Burundi ina wanajeshi 400 katika kikosi cha AMISOM na wengine ni wa Uganda.

Kutathimini changamoto inayokabili vikosi hivyo, na nini jumuiya ya kimataifa inaweza kuwasaidia wanajeshi hao Muandishi wetu wa Bujumbura, Ramadhani Kibuga amezungumza na Mkuu wa Majeshi ya Burundi Meja Jenerali Godfroid Niyombare anayefafanua kwanza hali halisi inayovikabili vikosi hivyo.

(MAKALA NA RAMADHANI KIBUGA)