Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uingizaji haramu wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa unatishia utulivu Guinea-Bissau

Uingizaji haramu wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa unatishia utulivu Guinea-Bissau

Usafirishaji haramu wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa vinasalia kuwa tishio kila wakati la utulivu nchini Guinea-Bissau, taifa ambalo ni miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani.

Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Joseph Mutaboba, alhamisi alipokuwa akitia taarifa kwenye Baraza la Usalama.

Bwana Mutaboba amesema kuna shuku kwamba baadhi ya majeshi yenye silaha nchini Guinea-Bissau yanashirikiana na mtandao wa uhalifu wa Amerika ya Kusini ili kuingiza kinyemela Ulaya dawa za kulevya aina ya cocaine kwa kupitia taifa hilo la Afrika ya Magharibi.

Bwana Mutaboba amesema mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa mihadarati nchini Guinea-Bissau ni changamoto kubwa kwani vita hivyo vinakabiliwa na vikwazo vingi vya kitaifa, siasa za nje na masuala ya kiufundi.

Ameongeza kuwa ukosefu wa takwimu sahihi za kiasi gani cha mihadarati kinachopitia nchini humo pia kinaongeza ugumu wa kushughulikia tatizo hilo.