Teknolojia ya nyuklia ina jukumu muhimu nchini Nigeria

3 Novemba 2011

Teknolojia ya nyuklia ina jukumu muhimu hasa la kukidhi mahitaji ya haraka ya watu nchini Nigeria, amesema naibu mwakilishi wa taifa hilo kwenye Umoja wa Mataifa.

Balozi Bukun-Olu Onemola akizungumza kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati baraza hilo likiendelea kujadili ripoti ya shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA amesema, ajali iliyotokea kwenye kinu cha nyuklia cha Fukushima Daiichi nchini Japan mapema mwaka huu imezusha mjadala wa kimataifa kuhusu uhalali wa umilikaji wa nguvu za nyuklia.

Hata hivyo balozi Onemola amesema nguvu za nyuklia ni kiungo muhimu katika mstakhabali wa Nigeria kwani taifa hilo linaamini kwamba ikitumika vyema, kwa usalama na kuzingatia misingi inaweza kusaidia watu kupata maendeleo na kutimiza malengo ya milenia. Ameongeza kuwa Nigeria ina ajenda ya kutumia nishati ya umeme ya nyuklia katika mikakati ya kitaifa ya kuleta mabadiliko na imesalia miaka michache tu kabla ya mwaka 2015 hivyo kwao nyuklia ni chachu ya kutimiza malengo ya kuwatoa watu katika umasikini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud