Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani ikizuia msaada kwa UNESCO shughuli nyingi zitaathirika:Bokova

Marekani ikizuia msaada kwa UNESCO shughuli nyingi zitaathirika:Bokova

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Iriba Bokova amesema katika wakati huu wa msukosuko wa kichumi na mabadiliko ya kijamii anaamini kwamba kazi muhimu ya UNESCO ya kuchagiza utulivu na misingi ya demokrasia duniani ni moja ya mambo yanayopewa uzito na Marekani.

Bi Bokova amesema Marekani ni mshirika muhimu wa kazi za UNESCO na ikizuia ahadi yake ya fedha na michango mbalimbali ambayo inapaswa kutoa kwa sheria za Marekani basi hali hiyo itadhoofisha uwezo wa UNESCO na kuathiri juhudi za shirika hilo za kujenga jamii za uwazi na huru.

Ameongeza kuwa fedha zinazotolewa na Marekani kwa UNESCO zinasaidia katika masuala mengi ikiwemo kuendeleza vyombo vya habari huru na vya ushindani nchini Iraq, Tunisia na Misri, huku Afghanistan ikisaidia kuwafunza kusoma na kuandika maelfu ya maafisa wa polisi. Amesema kwa msaada wa Marekani haya yote yanawezekana na Marekani inatambua thamani ya kazi za UNESCO.

Amesema UNESCO ina matumaini kwamba Marekani itaendelea kuwa mwanachama wa shirika hilo na kwamba suluhisho la suala la ufadhili litapatikana, kwani kukata ufadhili na msaada wa fedha kutoka Marekani kutaathiri pakubwa kazi muhimu za UNESCO ikiwemo elimu, kupigania demokrasia na kupambana na itikadi kali. Ameliomba bunge na watu wa Marekani kutafuta njia ya kuendelea kuisaidia UNESCO katika kipindi hiki kigumu.