Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC na UNHCR watia saini muafaka kukabili usafirishaji haramu wa watu na wahamiaji

UNODC na UNHCR watia saini muafaka kukabili usafirishaji haramu wa watu na wahamiaji

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu na madawa UNODC leo wametia saini muafaka wenye lengo la kupambana na usafirishaji haramu wa watu na uingizaji haramu wa wahamiaji.

Muafaka huo uliotiwa sahihi na kamishina mkuu wa wakimbizi Antonio Guterres na mkuu wa UNODC Yuri Fedotov inaadhimisha ushiririkiano wa kwanza rasmi baina ya vitengo hivyo viwili vya Umoja wa Mataifa. Akizungumza katika utiaji saini huo mjini New York Bwana Guterres amesema kazi ya UNHCR ya kuwalinda wakimbizi na watu wengine wanaohitaji ulinzi wa kimataifa inaendelea kukabiliwa na changamoto ikiwemo mazingira mabaya, ukatili, usafirishaji haramu na uingizaji haramu mambo ambayo ni tishio kwa uwezo wa wakimbizi kupata hifadhi.

Naye mkurugenzi mkuu wa UNODC Yuri Fedotov amekaribisha muafaka huo na kusema unafungua njia ya kufanya kazi pamoja baina ya mashirika hayo. Ameongeza kuwa wajibu wa UNODC ni kukabiliana na uhalifu wa kupangwa kazi ambayo inakwenda sambamba na ile ya UNHCR ya kuwalinda wakimbizi. Amesema wahalifu hupenda kutumia fursa zozote wazipatapo mfano wakimbizi wanaotafuta hifadhi na kuataka kupata maisha bora wanaweza kuwa wahanga wa usafirishaji haramu au uingizwaji haramu wa watu na hivyo ni muhimu kwa vyombo hivi viwili kushirikiana kutoa msaada unaohitajika kwa wanaouhitaji.