Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa UNHCR wauawa katika shambulio Afghanistan

Wafanyakazi wa UNHCR wauawa katika shambulio Afghanistan

Leo asubuhi shambulio la kupangwa lililohusisha watu wa kujitoa muhanga kwenye mji wa Kandahar nchini Afghanistan limeuwa wafanyakazi watatu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na kujeruhi wengine wawili.

Shambulio hilo limefanyika katika eneo la ofisi za UNHCR. Katika taarifa iliyotolewa leo na kamishina mkuu wa wakimbizi Antonio Guterres, UNHCR inatafuta kuelewa mazingira ya shambulio hilo lakini ukweli ni kwamba wafanyakazi wameuawa na kujeruhiwa na operesheni za ofisi ya shirika hilo Kandahar zimevurugwa.

Guterres amesema tukio la leo ni pigo kubwa kwa UNHCR na familia za waliopoteza maisha na kujeruhiwa, pia linadhihirisha hatari kubwa inayowakabili wafanyakazi wa misaada nchini Afghanistan.