Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watu duniani imetimu bilioni 7:Ban

Idadi ya watu duniani imetimu bilioni 7:Ban

Idadi ya watu duniani leo imetimu rasmi bilioni 7 amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York katika hafla maalmu ya kusherehekea tukio hilo.

Ban amesema siku hii ya kutimiza watu bilioni saba sio kuhusu kuzaliwa kwa mtoto mpya au kizazi kipya bali ni siku ambayo inahusu watu wote wa dunia hii. Amesema idadi hiyo inafikia kukiwa na changamoto nyingi zinazoikabili dunia hivi sasa ikiwemo vita, njaa, maandamo na matatizo ya kiuchumi.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ban ameongeza kuwa usawa bado ni tatizo kubwa huku wachache wakiishi maisha ya fahari na wengi wakiwa katika dimbwi la umasikini uliokithiri. Amesema kuna maendeleo makubwa katika upande wa madawa lakini kina mama wanakufa kila siku wakati wa kujifungua na watoto wanakula kila siku kutokana na kunywa maji machafu.

Amesema mabilioni ya dola yanatumika kununua silaha badala ya kuwapa watu usalama, je hii ni dunia gani ambayo mtoto wa bilioni saba aliyezaliwa leo ataishi? Amehoji Ban akizitaka nchi zote kushikama kutatua matatizo haya yanayoikabili dunia.

Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la idadi ya watu duniani UNFPA Babatunde Osotimehin amesema dunia inahitaji mapinduzi ya kijani ili kuhakikisha usalama wa chakula cha kutosha kulisha watu bilioni saba.

(SAUTI YA BABATUNDE OSOTHMEHIN)

Amesema makadirio ya UNFPA yanaonyesha kwamba ifikapo 2030 zaidi ya nusu ya watu wote duniani wataishi mijini na mahitaji yao ni makubwa ya elim, afya, usalama, chakula na maji.