Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano mkuu wa UNESCO umepiga kura kuijumuisha Palestina katika uanachama

Mkutano mkuu wa UNESCO umepiga kura kuijumuisha Palestina katika uanachama

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO leo limepiga kura kwenye mkutano mkuu wa shirika hilo na kuijumuisha Palestina kama mwanachama wake mpya. Kura hiyo inaifanya Palestina kuwa mwanachama wa 195 wa UNESCO.

Wanachama 107 wamepiga kura kuunga mkono, 14 wamepinga na 52 hawakupiga kura kabisa. Kwa mujibu wa UNESCO uanachama wa Palestina utakamilika itakapotia saini na kuridhia katiba ya shirika hilo. Kujumuishwa uanachama wa UNESCO kwa mataifa ambayo sio wanachama kamili wa Umoja wa Mataifa kunahitaji kupendekezwa na bodi ya wakurugenzi ya UNESCO na theluthi mbili ya kura za kuunga mkono inahitajika .

Mkutano mkuu wa UNESCO unafanyika kila baada ya miaka miwili na unahudhuriwa na nchi wanachama na wawakilishi, watazamaji kutoka mataifa ambayo sio wanachama, mashirika ya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGO’s na kila mwanachama anakuwa na kura moja tu.