Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa mpya za matumizi ya maji kwa kilimo zitalinda usalama wa chakula

Taarifa mpya za matumizi ya maji kwa kilimo zitalinda usalama wa chakula

Ongezeko la idadi ya watu na kumomonyoka kwa mali asili kwenye bonde la mto Nile kunaleta hatari ya kuzuka kwa njaa na umasikini kwenye kanda hilo na hivyo mipango madhubuti ya kuzuia kuzuka kwa janga hilo inahitajika limesema shirika la chakula na kilimo FAO.

Onyo hilo limetolewa wakati FAO ikiwasilisha matokeo ya mradi wa miaka 10 katika kanda ya wanaotumia maji ya mto Nile ambao umefadhiliwa na serikali ya Italia kwa lengo la kutoa taarifa muhimu na nyenzo za mikakati kwa wakuu serikali na wanaosimamia mali ya asili ili waanze kubadili hali hiyo.

Idadi ya watu katika bonde la mto Nile hivi sasa ni milioni 200 na inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia kati ya 61 na 82 ifikapo 2030. imesema ripoti hiyo ya FAO iliyotolewa leo kwenye mkutano unaofanyika Kigali Rwanda. Miongoni mwa nchi zinazoshirikiana maji ya mto Nile ni Burundi, Congo DRC, Misri, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Tanzania, Sudan, Sudan Kusini na Uganda.