Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misitu inaweza kulisha walio na njaa duniani:UM

Misitu inaweza kulisha walio na njaa duniani:UM

Misitu inaweza kuwa na jukumu muhimu la kuilisha dunia kwa mazao yake kuanzia majani yenye vitamin hadi matunda na mizizi, kwa mujibu wa ushirikiano wa kimataifa wa ubia wa misitu CPF unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. CPF imezitaka serikali kuwekeza zaidi katika utunzaji na uhifadhi wa misitu.

Kwa mujibu wa CPF yenye wanachama 14 yakiwemo mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa, wakati huu ambapo watu bilioni moja wanakabiliwa na njaa, jukumu la misitu kutumika kutengeneza mbao lisifunike umuhimu wa mchango wa misitu katika kulisha jamii nyingi masikini duniani na matumizi makubwa ya kuni lazima yadhibitiwe.

Mkurugenzi msaidizi wa misitu katika shirika la chakula na kilimo FAO Eduardo Rojas-Briales amesema misitu na miti mashambani ni chanzo cha moja kwa moja cha chakula na kipato kwa zaidi ya watu bilioni moja katika nchi masikini. Ili kuendelea na faida hizi serikali na wadau wengine wa maendeleo lazima waongeze uwekezaji katika kusaidia udhibiti na uhifadhi wa misitu.

Akitoa mfano amesema India watu milioni 50 wanategemea misitu ili kuishi wakati Laos chakula cha msituni kinatumiwa na asilimia 80 ya watu wake wote milioni 6.4 .