Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwa UM miaka 66 iliyopita

Dunia imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwa UM miaka 66 iliyopita

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema dunia imepiga hatua kubwa tangu kuzaliwa kwa Umoja wa Mataifa miaka 66 iliyopita. Ban amesema siku chache kuanzia sasa dunia itamkaribisha mwanachama mpya ,mtoto atazaliwa na kuifanya idadi ya watu duniani kufikia bilioni 7. Ameongeza kuwa watakuwa watu bilioni saba wenye nguvu, kwani sasa watu wanaishi miaka mingi zaidi, watoto wengi wananusurika kifo, tuna amani zaidi na wengi wanaishi kwa kufuata utawala wa sheria.

Ameyasema hayo wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa, na amepongeza ujasiri wa watu kwani amesema mwaka huu umekuwa wa mabadiliko, watu kila mahali wanasimama kupigania haki zao na uhuru wa binadamu. Hata hivyo hatua zote hizi zilizopigwa ziko katika tishio kubwa, kutokana na msukosuko wa kiuchumi, ukosefu wa ajira, matatizo ya usalama na mabadiliko ya hali ya hewa.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ban ameongeza kuwa lazima dunia itambue kwamba wakati huu Umoja wa Mataifa unahitajika kuliko wakati mwingine wowote, katika maingiliano yanayoongezeka kila mtu anacho cha kuchangia na kufaidika watu wakifanya kazi pamoja ni muhimu watu bilioni saba kuungana kwa manufaa ya dunia.