Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kukua kwa asilimia 6:IMF

Uchumi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kukua kwa asilimia 6:IMF

Uchumi wa nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kukua kwa asilimia 6 mwaka 2012 kwa mujibu wa shirika la fedha duniani IMF.

Shirika hilo linasema ukuaji wa uchumi katika eneo hilo umesalia kuwa imara wakati nchi nyingi za kipato cha chini zilisongwa na matatizo ya kudorora kwa uchumi. Katika makadirio ya IMF yanasema nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la sahara zitaendelea kukua kwa wastani wa zaidi ya asilimia 5 mwaka huu na kuongezeka kwa uzalishaji katika mataifa hayo kuchangia kukua kwa uchumi mwaka 2012.

Hata hivyo shirika hilo linasema hali sio sawia katika nchi zote, kwani katika nchi za kipato cha chini uchumi utakuwa kwa asilimia 6, nchi za kipato cha wastani kama Afrika ya Kusini uchumi utakua kwa asilimia 3.5 pekee kwa mwaka huu. Shirika hilo pia limesema familia masikini zimeathirika sana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta na njaa iliyolikumba eneo la Pembe ya Afrika.