Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani watatu wa UNAMID wauawa Darfur

Walinda amani watatu wa UNAMID wauawa Darfur

Walinda amani watatu wa mpango wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika kulinda amani Darfur Sudan UNAMID wameuawa usiku wa kuamkia leo kwenye shambulio katika kambi ya wakimbizi wa ndani.

Ukithibitisha mauaji hayo mpango wa UNAMID umesema askari hao walikuwa katika shughuli za kila siku za kushika doria waliposhambuliwa na kundi la watu wenye silaha majira ya saa mbili usiku saa za Sudan kwenye kambi ya Zam Zam iliyoko nje kidogo ya mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini wa El Fasher.

Majina ya marehemu bado hayajatajwa lakini UNAMID inasema wawili walikuwa askari na mmoja mshauri wa polisi, walinda amani wengine sita walijeruhiwa kwenye shamblio hilo.

Ibrahim Gambari mkuu wa UNAMID amelaani vikali shambulio hilo na kusema walinda amani hao walikuwa wakijaribu kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye kambi ya Zam Zam na ameitaka serikali ya Sudan kufanya uchunguzi mara moja ili kubaini walioendesha shambulio hilo na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.