Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya wanawake haukubaliki duniani:Manjoo

Ukatili dhidi ya wanawake haukubaliki duniani:Manjoo

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Rashida Manjoo amesema kuota mizizi na kusambaa kwa ukatili dhidi ya wanawake ni sala lisilokubalika popote dniani.

Akihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo Bi Manjoo amewasilisha ripoti ya katili huo, chanzo chake na athari zake. Amesema haijalishi unatokea wakati gani uwe wa amani au wa vita, mifumo ya ukatili dhidi ya wanawake inasababisha athari kubwa za ubaguzi, kutokuwepo usawa na ukandamizaji.

Ripoti hiyo imetoa tathimini ya mtazamo wa Bi Manjoo na wawakilishi wengine wawili waliomtangulia ambao wamepewa jukumu la kufuatilia na kutoa ripoti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya wanawake duniani.

Ripoti hiyo inabainisha mifumo ya ukatili na hatua gani zichukuliwe na serikali kukabiliana nayo kwani imesisitiza ukatili wowote dhidi ya wanawake ni ukiukwaji wa haki za kimataifa za binadamu.

Bi Manjoo amerejea wito wake kwa serikali zote kutimiza wajibu wao katika kutekeleza haki za binadamu kwa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, kuchunguza na kuwachukulia hatua wote wanaotekeleza vitendo hivyo. Pia amesema ni muhimu kuwalinda wanawake hao na kutoa msaada kwa waathirika wa ukatili.