Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio kulaani Syria

Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio kulaani Syria

Baraza la Usalama jumanne usiku limeshindwa kupitisha azimio ambalo lingelaani ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea nchini Syria, azimio ambalo lingeonya kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad ikiwemo vikwazo endapo hali hiyo ingeendelea.

Azimio hilo limeshindwa kupitishwa kutokana na kura mbili za turufu kutoka kwa wanachama wawili wa kudumu wa baraza hilo ambao ni Uchina na Urusi, kura tisa ziliunga mkono na wajumbe wane hawakupiga kura ambao ni Brazil, India, Lebanon na Afrika ya Kusini. Urusi na Uchina wametumia kura ya turufu kwa madai kwamba vikwazo sio suluhu na kwamba uongozi wa Syria unahitaji kuhusishwa kwenye mazungumzo. Balozi wa Marekani Susan Rise amepinga vikali kura hizo za turufu.

(SAUTI YA SUSAN RICE)

Balozi wa Ufaransa Gerard Araud ambaye nchi yake ndio ilioandaa azimio hilo amesema kura ya turufu imeonyesha kutojali uhalali wa yale yanayopiganiwa Syria. Hii ni kura ya kwanza ya turufu ya Uchina na Urusi tangu wote walipopiga kura hiyo kupinga vikwazo dhidi ya utawala wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwaka 2008. Umoja wa Mataifa unasema watu 2700 wameuawa Syria tangu kuzuka machafuko.