Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa wa kijinsia katika sekta ya elimu ni chachu ya mafanikio:UM

Usawa wa kijinsia katika sekta ya elimu ni chachu ya mafanikio:UM

Umuhimu wa kuwapa elimu bora wasichana na wavulana ndio kiini cha siku ya kimataifa ya waalimu ambayo kauli mbiu yake mwaka huu ni “elimu kwa ajili ya usawa wa kijinsia”.

Siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka ni ya kuwaenzi mamilioni ya waalimu kote duniani ambao wamejitolea maisha yao kufundisha, watoto, vijana na watu wazima umesema ujumbe maalumu uliotolewa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hii, likiwemo la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, la watoto UNICEF, la maendeleo UNDP, la kazi ILO na lile la Education International.

Mashirika haya yanakumbusha kwamba ili kufikia lengo la elimu kwa wote na kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia mtazamo wa jinsia katika elimu lazima ushughulikiwe kwa kuanza na fursa ya wasichana kupata elimu. Denis Sinyono mratibu katika shirika la Education International anaeleza ni kwa nini kauli mbiu ya mwaka huu ni “waalimu kwa ajili ya usawa wa kijinsia”

(SAUTI YA DENIS SINYONO)

Oktoba 5 pia inaadhimisha siku mashirika ya UNESCO na ILO yalipotia saini mkataba unaohusu hali ya waalimu hapo mwaka 1966. Kimataifa wanawake ndio idadi kubwa ya waalimu katika ngazi ya elimu ya msingi ikiwa ni asilimia 62 na katika nchi zingine asilimia 99.