Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kubadili maneno kwa vitendo:Al-Nasser

Ni wakati wa kubadili maneno kwa vitendo:Al-Nasser

Mjadala wa kila mwaka wa viongozi wa dunia umekunja jamvi kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumanne usiku. Rais wa baraza amesema umewadia wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mjadala huo kwa vitendo, kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa, maendeleo endelevu, mabadiliko ya Umoja wa Mataifa hadi ombi la Palestina kuwa taifa mwanachama.

Nassir Abdulaziz Al-Nasser amesema kukusanyika pamoja ni mwanzo tu lakini kufanya kazi pamoja kutaifikisha dunia kunakotakikana wakati akiwaambia wajumbe wote 193 wa baraza hilo wakati wakihitimisha mjadala.

Mjadala huo umehusisha ushiriki wa wakuu wa nchi na serikali 111, pia makamu wa marais, mawaziri, maafisa wa serikali na mwana mfalme mmoja. Al-Nasser amesema bila ya shaka huu umekuwa ni mjadala wa kihistoria ukijadili masuala mbalimbali muhimu.

(SAUTI YA NASSIR Al-NASSER)

Jumla ya nchi wanachama 191 likiwemo taifa mwanachama mpya kabisa wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini na watazamaji watatu wameshiriki, isipokuwa Saudia na Seychelles ndio hawakuhudhuria mwaka huu.