Suala la nyuklia la Iran linaweza kutatuliwa kwa suluhu ya majadiliano:UM

24 Septemba 2011

Mvutano wa hali ya mipango ya nyuklia ya Iran unaweza kutatuliwa tu kupitia mjadiliano ya kisiasa ambayo yatarejesha imani ya kimataifa ya njia ya matumizi ya amani ya mipango hiyo amesisitiza katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Ban amekutana na Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad mjini New York kando na mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea na kujadili naye kuhusu masuala ya haki za binadamu, masuala ya kikanda na kimataifa ikiwemo matukio ya karibuni Mashariki ya Kati, Afghanistan, Iraq, Libya na Syria. Ban amesema ushirikiano wa Iran kwa kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama ni muhimu sana.

Iran imerejea mara kadhaa kusema kwamba mipango yake ya nyuklia ni ya amani kwa ajili ya kuzalisha nishati, lakini nchi nyingi zinasema mipango hiyo ni ya kutaka kutengeneza silaha za nyuklia na mwaka jana Baraza la Usalama liliweka awamu ya nne ya vikwazo dhidi ya mipango hiyo ya Iran na hasa kwa kushindwa kutoa ushirikiano unaohitajika kwa shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter