Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awasilisha ombi la Palestina kwa Baraza la Usalama

Ban awasilisha ombi la Palestina kwa Baraza la Usalama

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepeleka ombi la Palestina la kutaka kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama ili lifikiriwe baada ya kupokea ombi hilo siku ya Ijumaa kutoka kwa Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmod Abbas. Ban amesema amewasilisha ombi hilo kwa balozi Nawaf Salam wa Lebanon ambaye ndio rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu. Palestina hivi sasa ina hadhi ya kuwa mtazamaji tu kwenye Umoja wa Mataifa.

Ombi lolote la uanachama linafikiriwa na Baraza la Usalama ambalo linaamua endapo kupendekeza ombi hilo au la, kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe 193, ambao watahitaji kupitisha azimio la kuidhinisha uanachama. Bwana Salam amesema atakutana na wajumbe wa Baraza la Usalama Jumatatu kufanya majadiliano ya ombi hilo la Palestina.