Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zahma ya Somalia ni aibu kwa dunia:Uturuki

Zahma ya Somalia ni aibu kwa dunia:Uturuki

Waziri mkuu wa Uturuki ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kuisaidia Somalia kumaliza janga la kibinadamu na kuleta amani na utulivu akisisitiza kwamba dunia haiwezi kuacha kilio cha taifa hilo la Pembe ya Afrika kikapita bila kusikilizwa.

Waziri huyo Tayyip Erdogan ameuambia mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba sasa hivi jumuiya ya kimataifa inayaangalia mateso ya Somalia kama sinema, lakini inapaswa kukabiliana nayo haraka hali ambayo ni mtihami mkubwa kwa utu wetu.

Bwana Erdogan amesema ameshuhudia kwa macho machungu ya watu wa Somalia alipozuru taifa hilo lililoghubikwa na vita mwezi uliopita.Amesema hakuna atakayezungumzia amani, haki na ustaarabu duniani wakati kilio cha Wasomali hakisikiki.

Uturuki imezindua kampeni ya msaada kwa Somalia na kukusanya dola milioni 300 katika miezi miwili iliyopita, pia iliaandaa mkutano wa dharura wa nchi za jumuiya ya kiislam OIC ambapo ahadi za zaidi ya dola milioni 350 zimetolewa.