Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia maradhi yasiyo ya kuambukiza ni rahisi kuliko kutibu:Ban

Kuzuia maradhi yasiyo ya kuambukiza ni rahisi kuliko kutibu:Ban

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuzuia maradhi yasiyo ya kuambukiza yaani NCD’s kama ugonjwa wa moyo, saratani, kisukari na maradhi ya kupumua ni raisi kuliko kutibu ambayo ni gharama kubwa. Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa maradhi yasiyo ya kuambukiza kwenye mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa hapa New York Ban amesema mkutano huu ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila watu watatu kati ya watano duniani wanakufa na magonjwa ambayo yanajadiliwa.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na maradhi haya ni muhimu sana kwani NCD’s ni tishio kubwa la maendeleo, na sasa yameanza kuwaathiri watu masikini na kuwatumbukiza zaidi kwenye dimbwi la ufukara. Mamilioni ya watu wanakufa kila mwaka na maradhi haya na wengi hivi sasa wako katika nchi zinazoendelea. Ban amesema nchi zote wanachama zina jukumu kubwa, hali ni ya hatari na wanajua nini kinapaswa kufanyika.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Bi Margaret Chan ambaye amesungumza pia kwenye mkutano huo wa vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vitaongezeka kwa asilimia 17 katika muongo ujao na barani Afrika idadi hiyo itafikia asilimia 24. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ni miongoni mwa viongozi wa Afrika waliohutubia mkutano huo. Anasema familia nyingi hasa masikini zinajikuta zikilemewa sana pale mmoja katika familia anapopatwa na maradhi hayo kwani ni gharama kubwa kuyatibu.

(SAUTI YA RAIS MUGABE)