UM wasifu ukomavu wa kidemokrasia Sierra Leone wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani

13 Septemba 2011

Mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika Magharibi amesifu ustamilivu na ukomavu wa kidemokrasia unaoendelea kujiri nchini Sierra Leone, lakini hata hivyo ameonyesha wasiwasi wake kufuatia mkwaruzano wa kisiasa ulioibuliwa na kambi mbalimbali za kisiasa ambazo huenda zikatio dosari maandalizi yaa uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Akizungumza kwenye baraza la usalama Michael von der Schulenburg amesifu hatua zinazoendelea kupigwa na wananchi wa taifa hilo ambao amewaelezea kama watu waliopevuka na kukomaa kisiasa na wameudhihirishia ulimwengu jinsi walivyopiga hatua kwenye ujenzi wa demokrasia. Hata hivyo amesema kuwa mkwamo uliojitokeza hivi karibuni baina ya wafuasi wa viongozi wa vyama vya kisiasa waliokwaruzana hadharani kuwa ni kitendo kinachoweza kuuweka kwenye majaribu makubwa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Amewataka wananchi pamoja na wafuasi wa vyama vya siasa kuliza chini jazba zao ili kuidumisha amani iliyopatikana katika kipindi cha miaka minane iliyopita.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter