Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu lateua jopo kuchunguza vitendo vya ukandamizaji wa serikali ya Syria

Baraza la haki za binadamu lateua jopo kuchunguza vitendo vya ukandamizaji wa serikali ya Syria

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limewateua maafisa watatu wataoendesha uchunguzi kuhusiana na nyenendo za utumiaji wa nguvu za kijeshi dhidi ya raia wanaoandamana nchini Syria.

Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa, tangu serikali izidishe operesheni zake za kijeshi kwa ajili ya kuwadhibiti waandamanaji hao watu wanaopoteza maisha wameongezeka hadi kufikia 2,600.

Jopo hilo la wataalamu litaongozwa na Sergio Pinheiro kutoka Brazil linatazamia kuendesha uchunguzi wake kuhusiana na uvunjifu wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na serikali katika kipindi cha kuanzia mwezi March mwaka huu pale yalipoanza kuzuka maandamano hayo.

Baraza hili la haki za binadamu lenye makao yake makuu mjini Geneva, hivi karibuni lilipitisha azimio la kuwapeleka wataalamu wake kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kufuatia taarifa za ripoti za awali kudai kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.