Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waanza kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu Libya

UM waanza kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu Libya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameanza kuweka zingatio la utoaji wa misaada ya dharura kwa mamia ya wananchi wa Libya ambao wanakabailiwa na uhaba wa mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula. Tayari shirika la mpango wa chakula duniani WFP limetuma tani kadhaa za chakula na misaada mingine ya kibinadamu ikiwemo madawa na nishati ya mafuta mjini Tripoli.

WFP pia imeanza kuratibu mkakati wa usambazaji chakula kwa makundi ya watu waliohatarini katika mji wa Tripoli na kwenye eneo lote la pwani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA limesema kuwa mji mkuu wa Tripilo na maeneo yanayopakana na Tunisia yanakabiliwa na mkwamo mkubwa wa ukosefu wa maji. Hali hiyo huenda ikawaathiri zaidi ya watu milioni nne.

Shirika la UNICEF limeanza kusambaza huduma za maji kwa baadhi ya maeneo mjini Tripoli lakini hata hivyo hali bado ni mbaya.