Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahusika wa mashambulio ya bomu Abuja lazima wapelekwe mbele ya sheria: Migiro

Wahusika wa mashambulio ya bomu Abuja lazima wapelekwe mbele ya sheria: Migiro

Naibu Katibu Mkuu wa UM Bi Asha Rose Migiro amelaani vikali mashambulio yaliyolenga majengo ya Umoja wa Mataifa nchini Nigeria. Asha –Rose Migiro aliwasili Abuja mwishoni mwa wiki - pamoja na Gregory Starr, mkuu wa idara ya usalama ya Umoja wa Mataifa kujionea uharibifu uliosababishwa na tukio hilo ambako watu kadhaa walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa..

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo lenye majengo ya Umoja wa Mataifa na kutembelea waliojeruhiwa kwenye hospitali ya Abuja, Bi Migiro alisisitiza kwamba hili ni shambulio dhidi ya wafanyakazi waliokuwa wakisaidia wananchi wa Nigeria.

Kushambulia watu kama hawa ni jambo la kusikitisha na lisilokubalika amesema Bi Migiro na kuongeza kwamba kitendo hicho hakitazuia UM kuendelea na kazi yake. Naibu Katibu Mkuu, ambaye alikutana na Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan kujadili mashambulizi haya, alisema wahusika lazima wapelekwe mbele ya sheria.  Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa umeanzishwa juu ya mashambulio haya yalioyolaaniwa na  Katibu Mkuu Ban pamoja na Baraza la usalama.