Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM ataka tathimini baada ya Marekani kuhusika na ukiukaji wa haki

Mtaalamu wa UM ataka tathimini baada ya Marekani kuhusika na ukiukaji wa haki

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya ukatili dhidi ya wanawake, sababu zake na athari zake Rashida Manjoo ameitaka serikali ya Marekani kuzipitia upya sera zake zinazohusika na ukatili dhidi ya wanawake. Wito wake unafuatia maamuzi ya tume ya Marekani ya haki za binadamu kubaini kwamba serikali ya Marekani inawajibika na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Bi Jessica Lenahan Gonzales ambaye ni muathirika wa ukatili dhidi ya wanawake na aliyepoteza watoto wake watatu.

Bi Manjoo amesema ukatili dhidi ya wanawake ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ambao unaendelea kutoa changamoto kwa kila nchi duniani na Marekani ni miongoni mwao. Ameongeza kuwa Marekani lazima itathimini upya njia za kuwalinda waathirika wa ukatili na kuwachukulia hatua wanaotekeleza ukatili huo dhidi ya wanawake. Pia inapaswa kuanzisha viwango vipya vya hatua za kuwalinda waathirika na kuweka adhabu kwa wasiotekeleza viwango hivyo.

Amesema ili kutimiza lengo hilo serikali inapaswa kuwa na mjadala kuanzia ngazi za chini hadi taifa na kuwashirikisha pande zote, kwa nadharia na vitendo, jambo ambalo litasaidia kuundwa sera, watu kukamatwa, kufunguliwa mashitaka, kuhukumiwa na kuwepo kwa program maalumu za kuelimisha jamii. Amesema ingawa sheria ipo Marekani lakini haiwabani kisheria wahusika wa ukatili na hivyo mara nyingi hawachukuliwi hatua kali.