Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brazil yatakiwa kuwalinda majaji wake, kufuatia kuuawa kwa jaji mmoja

Brazil yatakiwa kuwalinda majaji wake, kufuatia kuuawa kwa jaji mmoja

Umoja wa Mataifa umeitaka Brazil kuhakikisha inatoa ulinzi wa kutosha kwa watendaji wake wa kwenye baraza la maamuzi ikiwemo majaji, mahakimu na maafisa wengine, kufuatia tukio la kuuliwa kwa jaji mmoja aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana.

Jaji huyo Patrícia Lourival Acioli alipigwa risasi hadi kufa katika eneo karibu na nyumbani kwake huko Rio de Janeiro. Kufuatia kisa hicho, mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Gabriela Knaul amesema kuwa mamlaka za Brazil zinapaswa sasa kuangalia namna ya kuwalinda watendaji wake.

Ameitaka serikali hiyo kuhakikisha inachukua hatua za haraka ili kuwahakikishia usalama watendaji wake hasa wale walioko kwenye vyombo vya maamuzi. Jaji huyo aliyeuawa, alikuwa mstari wa mbele kukabiliana na makundi korofi, pamoja na maafisa wa polisi waliojihusisha na vitendo vya rushwa.