Operesheni za kijeshi dhidi ya raia zinaendelea Syria:UM

22 Agosti 2011

Uongozi wa Syria unaendelea kutumia nguvu za kijeshi kuwatawanya watu wanaoandamana kwa amani amesema kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay. Amesema watu takriban 40 wameuawa kati ya Alhamisi na Ijumaa iliyopita na mauaji hayo yametekelezwa na majeshi ya ulinzi na usalama ya Syria, siku moja tu baada ya Rais wa nchi hiyo Al Assad kumuhakikishia Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon kwamba hakuna tena operesheni za kijeshi dhidi ya raia.

Akihutubia baraza la haki za binadamu mjini Geneva hii leo kwenye kikao maalumu kuhusu hali ya Syria Bi Pillay amesema zaidi ya watu 2000 wameuawa tangu kuzuka kwa maandamano katikati ya mwezi March huku watu zaidi ya 350 wamearifiwa kuawa nchini humo tangu kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Ameongeza kuwa serikali lazima itimize ahadi yake ya kusitisha matumizi ya nguvu za kijeshi kuwakandamiza watu wanaoandamana kwa amani na kuwaachilia wote inaowashikilia kwa sababu ya kushiriki maandamano.

(SAUTI YA NAVI PILLAY)

Mswaada wa azimio uliowasilishwa kwenye baraza la haki za binadamu unalaani vikali hatua ya serikali ya Syria kuwashambulia raia wake na umeitaka serikali kuruhusu mazungumzo ya kitaifa yatakayojumuisha wote katika mazingira huru bila woga wala vitisho.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud