Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aendelea kumuasa Rais Assad kuhusu machafuko Syria

Ban aendelea kumuasa Rais Assad kuhusu machafuko Syria

Wakati huohuo katika mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Bashar Al-assad wa Syria hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon ameelezea hofu yake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia nchini humo.

Ban amesema vitendo vya ukiukwaji vinavyofanywa na majeshi ya ulinzi na usalama ya serikali vinaendelea katika wilaya za Al Ramel na Latakia ambako ni makazi ya maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina. Ban amesisitiza kuwa operesheni zote za kijeshi na kamatakamata lazima isitishwe mara moja nchini humo. Kwa upande wake Rais Assad amemuhakikishia Ban Ki-moon kuwa operesheni za jeshi na polisi zimesita.

Ban pia amerejea wito wa kufanyika uchungunzi huru dhidi ya ripoti zote za mauaji na vitendo vya ghasia na ameitaka serikali kutoa fursa kwa vyombo vya habari na kutoa ushirikiano kwa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. Amemtaka Rais Assad kujihusisha na mchakato wa amani ili kuelekea mabadiliko nchini humo.