Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Nitakuwa pale ninapohitajika”: wasema wafanyakazi wa UM katika maeneo wanayotoa huduma:

“Nitakuwa pale ninapohitajika”: wasema wafanyakazi wa UM katika maeneo wanayotoa huduma:

Dr wa Kimisri nchini Somalia Domar Saleh alikuwa anaishi maisha ya amani na ya kawaida kama mtaalamu wa upasuaji na mkufunzi wa chuo kikuu nchini Misri wakati alipopokea simu kutoka shirika la afya duniani WHO na kuambiwa madaktari wanahitajika haraka nchini Somalia, na hakufikiria mara mbili.

Dr Saleh leo wakati Umoja wa Mataifa ukijiandaa na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa hisani hapo Ijumaa Agosti 19 amesema “lazima niwe pale ninapohitajika, hivi ni vita na athari ziko kila mahali, lazima niwe pale”

Dr Saleh mwenye umri wa miaka 41 ameoa, ni baba wa watoto wawili, alisoma katika chuo kikuu cha Cairo na Ismaili ya Misri na kisha chuo kikuu cha madaktari cha Royal college of Surgeons mjini London, Uingereza. Ni miongoni mwa maelfu ya wafanyakazi wa hisani ambao juhudi zao za kupindukia zinasherehekewa kila mwaka Agosti 19.

Dr Saleh amesema akiwa Somalia ameshuhudia mengi ya kutia machungu na kutisha hasa kutokana na miaka 20 ya vita vya taifa hilo kutokuwa na serikali maalumu. Tangu 2007 amehudumu Baidoa Kusini na Kaskazini mwa Somalia na sasa yuko Moghadishu. Maelfu ya watu wameuawa, kujeruhiwa na kukimbia makazi yao Somalia tangu kuangushwa utawala wa Siad Barre zaidi ya miaka 20 iliyopita na kuzusha vita.