Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa ombi jipya la ufadhili kwa huduma zake kwenye pembe ya Afrika

UNHCR yatoa ombi jipya la ufadhili kwa huduma zake kwenye pembe ya Afrika

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetoa wito mpya wa kutolewa kwa ufadhili utakaolisaidia kutoa huduma za kibinadamu kwenye pembe ya Afrika. Hii ni baada ya njaa na ghasia zilinazoshuhudiwa, zinapoendelea kuchochea kuhama kwa watu ndani na kwenda nje mwa Somalia.

UNHCR kwa sasa inasema kuwa inahitaji dola milioni 144 ili kutoa huduma za dharura nchini Somalia , Ethiopia na Kenya ikiwa ni ongezeko la dola milioni 8.6 kutoka kwa ombi ililotoa mapema mwezi Julai mwaka huu. Hadi sasa UNHCR imepokea dola milioni 59 kutoka kwa wafadhili kwa oparesheni zake za dharura ikimaanisha kuwa UNHCR bado inahitaji dola milioni 86 kabla ya mwisho wa mwaka huu. Mwaka huu pekee UNHCR imesambaza misaada ya dharura kwa zaidi ya watu 100,000 kusini na kati kati mwa Somalia ambapo kulishuhudiwa hali mbaya ya ukame.