Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bi. Valeria Amos atembelea eneo la Kisomali nchini Ethiopia

Bi. Valeria Amos atembelea eneo la Kisomali nchini Ethiopia

Naibu katibu katika masuala ya kibinadamu na huduma za dharura kwenye Umoja wa Mataifa Valeria Amos amesema kuwa misaada zaidi ya kibinadamu inahitajika  kwenye eneo la Kisomali nchini Ethiopia pamoja na usalama kwa watoa huduma za kibinadamu katika eneo hilo. Bi Amos alisafiri kwenda mji mkuu wa eneo hilo Jigiga kukutana na rais wake Abdi Ilie na maafisa wengine.

Akipongeza hatua ambazo zimechukuliwa na utawala wa eneo hilo, Bi. Amos hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuwahakikishia wafanyikazi wa kutoa huduma za kibinadamu katika eneo hilo na kuwasaidia wanaohitaji misaada. Amesema kuwa kwa miaka michache iliyopita huduma za kibinadamu katika eneo hilo la Kisomali zimeathirika kutoka na ukosefu wa usalama. Amos pia ametembelea eneo la Bisle Kebele ambapo amezuru vituo vya afya.