Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wengi duniani bado wanapitia mateso na ukosefu wa usawa :UM

Wanawake wengi duniani bado wanapitia mateso na ukosefu wa usawa :UM

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inayotoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwepo kwa usawa wa kijinsia inasema kuwa mamilioni ya wanawake kote duniani bado wanaendelea kukumbwa na ukosefu wa haki na usawa kazini, manyumbani mwao na kwenye maisha ya kawaida.Ripoti hiyo ndiyo ya kwanza ya wanawake wa Umoja wa Mataifa iliyozinduliwa mapema mwaka uliopita yenye lengo la kuunga mkono Umoja Wa Mataifa katika kupigania usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa hata kama nchi 139 tayari zimejumuisha usawa wa kijinsia kwenye katiba zao bado wanawake wanazidi kupitia dhuluma wakiwa nyumbani na kwenye maeneo ya kufanyia kazi. Pia inaongeza kuwa huku dhuluma za nyumbani zikiwa zimepigwa marufuku kwenye nchi 125 bado wanawake milioni 603 wanaishi kwenye nchi ambapo dhuluma hizo hazitambuliwi kama makosa.