Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM kuweka jeshi la mda kwenye jimbo linalozozaniwa la Abyei Sudan

UM kuweka jeshi la mda kwenye jimbo linalozozaniwa la Abyei Sudan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubaliana kuanzisha jeshi la muda kwenye jimbo la Abyei linalozozaniwa nchini Sudan. Jeshi la Umoja wa Mataifa la usalama kwa ajili ya Abyei UNISFA litakuwa na wanajeshi 4200 na maafisa wa polisi 50, pamoja na walinda amani wa kiraia. Mpango huo wa kulinda amani utasaidia kufanikisha makubaliano ya hatima ya jimbo la Abyei, pia utatumika kama kiungo cha amani baina ya pande mbili za mpaka.

Philip Parhan ni naibu balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa anasema kwanza ni muhimu sana pande zote zikatimiza wajibu wake chini ya makubaliano ambayo yanajumuisha kuondoa majeshi ya Sudan, SPLA na majeshi mengine washirika kutoka jimbo la Abyei haraka iwezekanavyo.

Pili amesema ni muhimu kuondokana na muafaka wa muda ,kwani zimesalia wiki mbili tuu kabla ya Julai 9 ambao Sudan Kusini inakuwa taifa huru rasmi na pande zote zinahitaji kutatua masuala ambayo bado yanatatiza chini ya mkataba wa amani wa CPA likiwemo suala la hatma ya Abyei na mengine kama mapato ya mafuta, uraia na mpaka.