Waziri wa zamani wa Rwanda afungwa maisha na mahakama ya ICTR

24 Juni 2011

Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda ICTR iliyoko Arusha Tanzania leo imemuhukumu kwenda jela maisha mwanamke wa kwanza kushitakiwa kwenye mahakama hiyo.

Mwanamke huyo Pauline Nyiramasuhuko aliyekwa waziri wa zamani wa masuala ya familia amekutwa na hatia ya kupanga mauaji ya kimbari na kuratibu ubakaji wa wanawake na wasichana wakati wa mauaji hayo mwaka 1994 nchini Rwanda.

Bi Nyiramasuhuko mwenye umri wa miaka 65 na mtoto wake wa kiume Arsene Shalom Ntahobali walikuwa wanakabiliwa na mashitaka 11, yakiwemo mauaji, ubakaji na utesaji wa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Mahakama imeelezwa kwamba waziri huyo wa zamani na familia yake walishiriki kuunda vikundi vya wanamgambo waliotekeleza mauaji na hasa Kusini mwa jimbo la Butare. Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani wapatao 800,000 waliuawa katika siku 100 za machafuko Rwanda mwaka 1994.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter