Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yamtaja mcheza filamu nyota Forest Whitaker kuwa balozi wake mwema

UNESCO yamtaja mcheza filamu nyota Forest Whitaker kuwa balozi wake mwema

Mcheza filamu na mtayarishaji mashuhuri wa Hollywood Forest Whitaker ametangazwa kuwa balozi mwema kwa ajili ya amani na maridhiano wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO.

Kazi zake zitajumuisha kusaidia kuelimisha watu na kuchagiza serikali kutoa kipaumbele kwenye programu za vijana zenye lengo la kuleta amani, elimu, haki za binadamu na masuala ya uraia wa kimataifa.

Akizungumza baada ya kutangazwa Whitaker amesema ana matumaini makubwa kwa sababu amekutana na watu wengi ambao wanajaribu kinua utu wa watu na kuleta maendeleo. Hivyo amesema matumaini yake ni kuwa na miradi mingi ya kuhamasisha vijana, kuwawezesha, na kuwaelimisha vijana.

Whitaker alishinda tuzo ya Oscar baada ya kucheza filamu  iliyotanabaisha maisha ya dikteta wa zamani wa Uganda Idi Amin iitwayo “The Last King of Scotland” . Pia alitayarisha filamu kuhusu askari watoto nchini Uganda iitwayo “Better Angels”.