Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kupata ripoti za ukiukaji wa haki ofisi ya haki za binadamu inataka uchunguzi ufanyike Syria

Baada ya kupata ripoti za ukiukaji wa haki ofisi ya haki za binadamu inataka uchunguzi ufanyike Syria

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina dhidi ya madai ya kusambaa kwa ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na serikali ya Syria wakati wa kuwasaka waandamanaji.

Ukiukaji huo ni pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi, kuwasweka mahabusu nautesaji.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay amesema ripoti hiyo pia imedai kutumiwa kwa risasi dhidi ya raia wasio na silaha,ambao unafanywa na askari wa serikali wakiwalenga waandamanaji kutokea kwenye mapaa ya majengo ya serikali na hasa kwenye maeneo yaliyo na mkusanyiko mkubwa wa raia. Ripoti ya ukiukwaji huo imeandaliwa na ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na imetolewa rasmi hii leo mjini Geneva.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo hadi kufikia sasa idadi ya walio uawawa inasemekana kuzidi 1100, wengi wa waliouawa ni raia wakiwemo wanawake na watoto.

Serikali ya Syria imekuwa ikikosolewa vikali kwa machafuko hayo dhidi ya waandamanaji ambayo ni sehemu ya mfumoko wa kudai haki za demokrasia uliojitokeza mwaka huu Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini , kuanzia Tunisia, Misri hadi Libya.