Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh, IOM zakubaliana kuwalipa fidia wafanyakazi waliokimbia Libya

Bangladesh, IOM zakubaliana kuwalipa fidia wafanyakazi waliokimbia Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uhamiaji IOM  kwa kushirikiana na serikali ya Bangladesh litaanza kuwafidia wafanyakazi walio raia wa nchi hiyo ambao wamelazimika kurejea nyumbani toka Libya kutokana na kukosekana kwa hali ya usalama.

IOM imeafiki kutoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 680 ambacho kitatumika kuwafidia wafanyakazi wapatao 36,000 waliokwisha rejea nyumbani. Lakini pia mpango mwingine uliosainiwa mapema mwezi uliopita unatazamiwa kuwasaidia pia raia wengine waliokuwa wakishughulisha katika nchi za Misri na Tunisia lakini wakaamua kurejea kutokana na kuvurugika kwa hali ya kisiasa.

Shughuli za kuanza kuwasaidia raia hao zinatazamiwa kuanza mwezi ujao wa July na wakati huo huo IOM itawajibika kuratibu na utunzaji wa kumbukumbu juu ya wale wote watakaofikiwa na msaada huo.