Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria yashutumiwa kujaribu kuwaangamiza raia wake

Syria yashutumiwa kujaribu kuwaangamiza raia wake

Serikali ya Syria imeshutumiwa kwa kujaribu kusitisha vuguvugu la raia wake kwa kutumia vifaru,mabuldoza na walinga shabaha. Kamishina mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay amesema ghasia dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani ni kinyume na ameitaka serikali ya Syria kusitisha mashambulizi dhidi ya raia wake. Pillay amesema ofisi yake imepokea ripoti za watu zaidi ya 1100 kuuawa tangu kuanza kwa maandamano mwezi Machi na wengine zaidi ya 10,000 wanashikiliwa.

Ameiomba serikali ya Syria kuruhusu tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuzuru nchi hiyo kama inavyotakiwa na baraza la haki za binadamu ili kupata ukweli na mazingira ya madai ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu.

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

Kamishina mkuu pia amelaani mauaji ya kijana wa miaka 13 Hamza al-Khatib ambaye inadaiwa alitekwa na kuteswa hadi kufa na majeshi ya usalama ya Syria . Pillay amesema mauaji ya kijana huyo ni ishara ya serikali kutumia kila njia kunyamazisha waandamanaji.