Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa UM azuru DR Congo
Naibu mkuu wa masuala ya kibinadamu na masula ya dharura wa Umoja wa Mataifa Catherine Bragg leo ameanza ziara ya siku tano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa lengo la kutanabaisha ulimwengu kuhusu moja ya matatizo makubwa na sugu ya kibinadamu nchini humo.
Suala la kulinda raia, kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kimapenzi na kupata fursa za kuwafikia wanaohitaji msaada katika maeneo ya vita ni muiongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele na naibu mratibu huyo wa OCHA atakapokutana na maafisa wa serikali, mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na jumuiya za kimataifa za misaada.
Nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya masuala ya kibinadamu na hali inakuwa mbaya zaidi ukichanganya na matatizo ya awali kama umasikini uliokithiri, usalama mdogo na ukatili dhidi ya raia ikiwemo mauaji na ubakaji.
Bi Bragg atazuru Kivu ya Kusini na jimbo la Oriantale , majimbo mawili kati ya yaliyoathirika zaidi na vita ili kukutana na jamii pia mashirika ya msaada wa kibinadamu na wadau wengine wa kimataifa walioko nchini humo.
Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 1.7 wa Kivu ya Kusini miongoni mwao 670,000 ni wakimbizi wa ndani kutokana na vita vinavyoendelea. Na katika jimbo la Oriantale maelfu ya watu na maisha yao wako katika hofu kutokana na uasi unaondeshwa na kundi la Uganda la LRA.